Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akisalimia wananchi baada ya kuwasili Peramiho. Kushoto kwake ni ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega akifuatiwa na Mratibu wa Kitivo cha Udaktari Peramiho Chuo cha Mt Augustino Tawi la Songea Padre Dunstan M. Mbano
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akikagua maeneo ya kitivo cha udaktari Peramiho. Kushoto kwake ni Joseph Joseph Mkirikiti na kulia kwake ni ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega akifuatiwa na Mratibu wa Kitivo cha Udaktari Peramiho Padre Dunstan Mbano



Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akielekezwa jambo na ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega.

Jengo la utawala ambalo bado halijaanza kutumika

Jengo la hosteli ya wanafunzi ambalo bado halijaanza kutumika
Jengo la Maabara Kitivo cha Udaktari Peramiho baada ya ukarabati ambalo bado halijaanza kufanya kazi kutokana na ukosefu wa vifaa vya kufundishia

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akihutubia wananchi wa Peramiho
Serikali imepongeza uamuzi wa Chuo Kikuu cha Mt Augostino Tanzania kuanzisha kitivo cha udaktari katika kituo chake cha Songea. Hayo yalisemwa jana tarehe 15.12.2012 na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ndugu Said Thabit Mwambungu alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya chuo hicho kilicho katika eneo la Peramiho.  Amesema kuanzishwa chuo hicho ni ukombozi kwa Mkoa wa Ruvuma ambao awali haukuwa na vyuo vya elimu ya juu.

“Kuanzishwa kwa chuo cha Tiba ni lulu kwa mkoa wa Ruvuma kwa vile kitapunguza usumbufu kwa wananchi wa ukanda huu ”alisema Mwambungu.

Aidha, akijibu risala ya chuo kuhusu tatizo la ardhi kwa ajili ya upanuzi wa eneo la chuo, Mwambungu amewataka watendaji walio chini yake wakae na uongozi wa chuo kwa ufumbuzi. Alisisitiza kuwa anaamini liko ndani ya uwezo wao.

“Watendaji kuanzia kijiji kaeni na viongozi wa chuo kupata ufumbuzi wa tatizo hili nanaamini hata likiwashinda, ofisi ya Mkuu wa Wilaya itawasaidia” alisema ndugu Mwambungu.

Akizungumzia tatizo la maji, amekemea tabia ya wananchi kuharibu mazingira na vyanzo vya maji na kusababisha tatizo la maji. Amewataka wananchi waache tabia hii mara moja. Akifafanua zaidi amewataka viongozi wa dini waisaidie serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tatizo la uharibifu wa mazingira na athari zake.

“Nawaomba viongozi wa dini mzungumze na waumini wenu kuhusu tatizo hili wakati serikali inasimamia sheria kuhusu waharibifu na uharibifu mazingira” Alisema Mwambungu.

Kwa upande wa umeme alisema watakaa na pande zote zinazohusika ili kupata ufumbuzi kwa vile linaigusa serikali pia.

Awali mratibu wa Kitivo cha Udaktari Peramiho Chuo cha Mtakatifu Agustino Tawi la Songea Padre Dunstan M. Mbano alisema Padre Mbano alisema chuo kina wanafunzi 39 wa mwaka wa kwanza wanaosoma masomo ya udaktari ambao wamelazimika kupelekwa kwa muda katika Chuo cha Ifakara-Morogoro kilicho chini ya Chuo Mama cha Mtakatifu Augustino wakisubiri kukamilika kwa miundo mbinu. Alisema, hata hivyo, wanafunzi hawa kiutawala bado wako chini ya Chuo Kikuu cha Mt Augustino Kituo cha Songea. Alisema Kituo cha Songea kilizinduliwa Novemba mwaka 2011 na kina jumla ya wanafunzi 631. Wanafunzi wa shahada ya kwanza ualimu kwa mwaka wa kwanza na wa pili ni 592 na wanaosoma udaktari ni 39.



Padre Mbano alisema ujenzi wa chuo umegawanyika katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ilihusu ukarabati wa majengo ya iliyokuwa hospitali ya wakoma, nyumba ya Mkuu wa Chuo, jengo la utawala na hostel kwa ajili ya wanafunzi. Awamu ya pili na tatu zitahusisha ujenzi wa hostel mbili, ukumbi, maktaba, ,adarasa na nyumba za walimu.

Padre Mbano alisema chuo kinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa umeme, maji na samani na vifaa vya kufundishia. Kuhusu umeme, alisema zinahitajika shilingi za Kitanzania milioni 178.3 kuufikisha umeme katika eneo hilo na kwa upande wa samani na vifaa vya kufundishia zinahitajika shilingi za Kitanzania milioni 57.3.

Habari na mwanablog
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top